INAUMA SANA! Baba aliyejulikana kwa jina moja la Mushi, mkazi wa Namanga- Msasani jijini Dar,
amemfanyia unyama wa kutisha mtoto wake wa kumzaa, (jina limehifadhiwa)
mwenye umri wa miaka 6, kwa kudaiwa kumfunga kamba mikononi na miguuni
kisha kumfungia ndani.
Habari za kusikitisha zilizofika kwenye meza ya gazeti hili zilidai
kuwa, baba huyo amekuwa na tabia ya kumfungia ndani mtoto huyo kuanzia
asubuhi mpaka jioni anaporudi kwenye kazi zake, jambo ambalo limekuwa
likiwaumiza majirani zake.
SHUHUDA AZUNGUMZA
Akizungumza na Uwazi, shuhuda wa tukio hilo
ambaye ni mmoja wa majirani wa baba huyo (jina linahifadhiwa)
aliliambia gazeti hili kuwa, mara nyingi walikuwa wakisikia sauti ya
mtoto akilia kwa muda mrefu kutoka ndani ya chumba cha baba huyo wakati
huohuo hawakuwa wanamuona mtoto Brian akicheza nje na wenzake kama
zamani.
Aliendelea kudai kuwa, kipindi cha nyuma baba huyo ambaye ametengana
na mama wa mtoto huyo, alikuwa akimfungia mwanaye ndani lakini akiondoka
mtoto huyo anafungua mlango na kujumuika na wenzake.
“Mara nyingi tunakuwa tunasikia mtoto analia ndani kwa muda mrefu
sana akisema ‘nakufaa… nisaidieni…’ na pia hatukuwa tunamuona akitoka
nje kucheza na wenzake kama zamani,” alidai jirani huyo na kuongeza:
“Unajua huyu baba anaishi na mtoto wake bila mama, sasa kila mara
anamfungia na kudai eti ni mtundu sana, anamshindisha njaa siku nzima,
sisi kama wazazi tulishangazwa sana na tabia hiyo.”
WATOTO WENZAKE NAO WANENA
Jirani huyo alisema watoto wao ndiyo walikuwa wakiwaambia mara kwa
mara kuwa mwenzao huyo anakatazwa na baba yake kucheza nao, hivyo
amekuwa akifungiwa ndani mchana kutwa.
WAZO LA KWENDA POLISI
Alisema siku ya tukio waligundua mtoto huyo kafungiwa ndani kama
kawaida baada ya kusikia akilia kwa muda mrefu akiomba msaada, ndipo
walipojikusanya na kuwa na wazo la kufikisha ishu hiyo polisi.
“Kwa kweli uvumilivu ulitushinda, tulimsikitikia sana yule mtoto,
tuliona anachofanyiwa tena na baba yake mzazi siyo sawa, hata kama ni
mtundu lakini hakustahili kufanyiwa ukatili huo, tulichoamua ikawa ni
kwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Oysterbay, nao bila hiyana
walifika eneo la tukio na kuona hali halisi.”
POLISI WAVUNJA MLANGO
“Kwa kufuata taratibu, polisi walivunja mlango na kumkuta mtoto huyo
akiwa uchi wa mnyama huku akiwa amefungwa kamba miguuni na mikononi kwa
nyuma na puani katapakaa kamasi na alionekana kutokwa na jasho jingi.
Inauma sana,” alisema jirani huyo.
Aliongeza kuwa, baada ya kuona hivyo kama wazazi waliumia sana na
kuamua kumsindikiza mtoto huyo katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay
jijini Dar wakiwa na polisi kwa uchunguzi zaidi.
BABA ATOWEKA
Shuhuda huyo aliongeza kuwa walipofika polisi waliambiwa jeshi hilo
litamsaka baba wa mtoto huyo, hata hivyo taarifa zinasema Mushi
aliposikia kwamba mwanaye amechukuliwa na polisi alitoweka mpaka leo
hajulikani alipo.
MAMA WA MTOTO AFUNGUKA
Gazeti hili lilipata fursa ya kuzungumza na mama wa mtoto huyo ambapo
alisema amewasili jijini Dar akitokea Moshi kuja kumchukua mwanaye
baada ya kusikia yanayompata kutoka kwa baba yake.
“Unajua mimi nilitengana na huyo baba yake muda mrefu, lakini cha
ajabu alimtuma mdogo wake kuja kumuiba huyu mtoto nyumbani kwetu.
“Baada ya mtoto huyo kuletwa Dar kwa baba yake nikawa napigiwa simu
na majirani zangu mara kwa mara na kuambiwa kuwa mwanangu anateseka
sana.
“Kama mama niliumia sana, nikaona nina kila sababu ya kuja kumfuata
ndipo nikamkuta polisi na kukabidhiwa huku baba yake akiendelea kusakwa.
“Inasikitisha, kwa nini alikuwa anamfunga kamba na kumfungia ndani?
Imeniuma sana. Nimekuja Dar kuja kumchukua mwanangu, hakika nimeumia mno
moyoni,” alisema mama huyo.
POLISI NAO WANENA
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, SACP Suzana
Kaganda hakuweza kupatikana jana lakini ofisa mmoja wa polisi wa
Oysterbay aliyeomba jina lake lisiandikwe gazetini kwa kuwa siyo
msemaji, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, akasema baba wa mtoto
huyo anatafutwa ili ajibu tuhuma hizo na upelelezi ukikamilika aweze
kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Ni unyama wa kutisha aliokuwa akifanyiwa huyu mtoto lakini polisi
tutahakikisha baba yake anakamatwa na sheria ichukue mkondo wake ili iwe
fundisho kwa wengine wanaowatesa watoto wao,” alisema ofisa huyo.
STORI: IMELDA MTEMA, DAR
No comments:
Post a Comment