Mahsein Awadh ’Dk. Cheni’ akiwa na jembe lake.
STAA mkubwa wa filamu za Kibongo, Mahsein Awadh ’Dk. Cheni’, amevamiwa
na watu wawili wanaodaiwa ni vibaka na kufanyiwa fujo, kisa kikidaiwa
kuwa ni dhamana aliyomwekea mwigizaji Elizabeth Michael ‘Lulu’ katika
ile kesi ya kifo cha Steven Kanumba.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, tukio hilo la kusikitisha lilijiri maeneo ya
Viwanja vya Leaders Kinondoni, Dar hivi karibuni wakati staa huyo
akitaka kuondoka eneo hilo.
Habari zilitonya kuwa vijana hao wakiwa na pikipiki (bodaboda)
walimfuata Dk. Cheni na kuanza kummwagia vitisho wakimhoji kwa nini
amekuwa ‘klozi’ sana na Lulu.
Bila kufafanua ukaribu wa mastaa hao wa filamu unawakera nini, wavamizi
hao walipasua vioo vya gari la Dk. Cheni aina ya Mitsubishi Pajero.
ILIKUWAJE HASA?
Shuhuda wetu alisimulia kuwa wakati wa tukio hilo Dk. Cheni na Lulu
hawakuwa pamoja, jambo lililomfanya msanii huyo kupigwa na butwaa asijue
la kuwajibu wale vijana na kuacha hatma yake mikononi mwa watekaji.
BAADA YA KUPASUA KIOO
“Walipopasua kioo cha mbele cha gari upande wa dereva, vijana wale
waliondoka na kumwacha Dk. Cheni akiwa hajui cha kufanya,” shuhuda
alisema.
Hata hivyo, inadaiwa wakati vijana hao wakimtaiti Dk.Cheni walisikika
wakitaja jina la Kanumba bila kufafanua anahusika vipi na kitendo chao
cha kumvamia msanii huyo.
Inaelezwa kuwa jitihada za msanii huyo kuwadhibiti wahalifu wale wa
amani hazikuweza kuzaa matunda na hivyo kumfanya nguli huyo wa filamu
kuhesabu hasara ya kioo hicho.
Steven Kanumba enzi za uhai wake.
DK CHENI ALIRIPOTI POLISI?
Amani lilipomuuliza ‘sosi’ huyo kama Dk. Cheni alikwenda kuripoti
polisi, jibu la swali hilo lilikuwa ni hapana, sababu ikiwa ni mtendwa
kushindwa kukariri namba za pikipiki.
“Alishauriwa aende polisi lakini akasema hawezi kufanya hivyo kwa sababu
wahusika hawafahamu na kwamba hana ushahidi wowote wa kuwafanya
watuhumiwa wakamatwe
HUYU HAPA DK. CHENI
Baada ya kupata taarifa hizo, Amani lilimsaka Dk. Cheni ambaye alikiri
kuvamiwa na watu hao na kupasua kioo cha gari lake lakini hawakumjeruhi.
“Kumekuwa na matukio mengi ya ajabuajabu yananitokea, nadhani hivi sasa
nitakuwa makini sana, nitaripoti polisi kila kitu, siwezi kuendelea
kupuuzia,” Dk Cheni alisema.
TUJIKUMBUSHE
Dk. Cheni alijitahidi kwa hali na mali kumsaidia Lulu kutoka gerezani
Segerea akikabiliwa na kesi ya kuua bila kukusudia katika kifo cha
Kanumba aliyefariki dunia Aprili 7, mwaka jana ambapo alisota kwa muda
wa takribani miezi kumi hadi alipotolewa kwa dhamana ya shilingi milioni
20, mwezi Machi mwaka huu.
Hivi karibuni Dk. Cheni alilazwa katika Hospitali ya Buruhani iliyopo
maeneo ya Posta, Dar, baada ya kula chakula kilichosadikiwa kuwa na
sumu. Matukio hayo yanazidi kuibua maswali mengi na akitakiwa kuwa
makini zaidi.
Elizabeth Michael ‘Lulu’.UHUSIANO WA DK. CHENI, LULU
Takribani miaka kumi iliyopita, Dk. Cheni alimfuata mama mzazi wa Lulu,
Lucresia Karugila akamuomba amwingize mwanaye kwenye sanaa ya uigizaji
katika Kundi la Kaole.
Dk. Cheni aliwahi kukiri kuwa mama Lulu alimkabidhi mwanaye awe baba
mlezi katika sanaa, kazi ambayo staa huyo aliifanya. Hivyo kitendo cha
kuwa ‘beneti’ na Lulu alipopata matatizo kilikuwa ni mwendelezo wa
malezi anayompatia hadi sasa.
KWA NINI LULU AMPONZE DK. CHENI?
Swali linalokosa jibu ni hili la kwa nini Lulu amponze Dk. Cheni wakati
huu akiwa uraiani ambapo baadhi ya wadau wa sanaa wamechangia mawazo kwa
kusema huenda ni wivu wa kimapenzi au roho mbaya.
“Unajua watu wengi wanataka kufanya kazi na Lulu, sasa wanapoona wanashindwa kumpata wanadhani Dk. Cheni anawabania.
“Lakini pia inawezekana watu wanapomuona Dk. Cheni na Lulu wako pamoja
wanadhani ni wapenzi, sasa kama Lulu alikuwa na mpenzi ni rahisi kuhisi
amepinduliwa,” alisema Jenista Aron msanii chipukizi mkazi wa Kinondoni,
Dar.
No comments:
Post a Comment