MFANYAKAZI
wa Jaji Kileo, Philemon Laiza (27) anadaiwa kumchinja mtumishi wa ndani
wa jaji huyo, ambaye ni raia wa Kenya, Perpetua Mainab (30).
Mtuhumiwa huyo, ambaye alikuwa ni mtunza bustani katika nyumba ya Jaji Kileo, alifanya unyama huo wiki iliyopita.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam jana, Kamishna wa Polisi Kanda Maalum, Suleiman
Kova, alisema mwili wa mtumishi huyo wa ndani ulikutwa kwenye dampo la
kutupia takataka maeneo ya Mikocheni B.
“Tukio
hilo lilitokea karibu na dampo la kutupia taka Mikocheni ‘B’, katika
eneo linalomilikiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
“Mfanyakazi
huyo wa ndani alikutwa ameshakufa baada ya mwili wake kuchinjwa sehemu
ya shingo, jeraha sehemu ya mkono wa kushoto karibu na kiganja, jeraha
kwenye paji la uso na mwili wake ukiwa umetapakaa damu sehemu za
kichwani,” alisema Kova.
Alieleza
kuwa mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa akifanya kazi pamoja na marehemu,
alikiri kuwa na marehemu siku hiyo ya Ijumaa ya Juni 8 mwaka huu.
Alisema
baada ya polisi kufanya upelelezi mtuhumiwa alikutwa na kiatu kimoja
cha marehemu na nguo alizovaa siku ya tukio, ambazo zilikuwa zimetapakaa
damu.
“Nguo hizo za marehemu zilikuwa zimetapakaa damu na baada ya mahojiano ya muda mrefu, mtuhumiwa alikiri kuhusika na tukio hilo.
Kamishna
Kova alisema kuwa mtuhumiwa alipohojiwa alidai kuwa marehemu alitoweka
nyumbani tangu siku ya Ijumaa na baada ya kubanwa na polisi mtuhumiwa
alikiri kuhusika na tukio hilo.
Kova alisema mtuhumiwa bado anahojiwa na upepelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani.
No comments:
Post a Comment