MATANGAZO

/zest+mkali+3.jpg /TULAMCHA+2+copy.jpg

Tuesday, 25 July 2017

ROLI LATUMBUKIA MTO WAMI WAWILI WAPOTEZA MAISHA

Image may contain: one or more people and outdoorMADEREVA wawili wa kampuni ya Usangu Logistics wamekufa baada ya gari la mizigo walilokuwa wakisafi ri nalo kutumbukia katika Mto Wami uliopo Chalinze, wilayani Bagamoyo.
Akizungumza jana mjini hapa, Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Jonathan Shana alisema ajali hiyo ilitokea usiku wa saa 7:00 kuamkia jana. Gari aina ya Scania lenye namba za usajili T857 ARP lililokuwa linatoka Dar es Salaam kwenda Arusha lilikatika breki na kugonga kingo za mto na kutumbukia mtoni.
Dereva aliyekuwa anaendesha gari hadi linatumbukia mtoni ametajwa kuwa ni Yahaya Karim anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 30 na 35. Alisema jina na mtu mwingine ambaye pia ni dereva, halikufahamika mara moja.
Matukio ya ajali yamekuwa mengi nchini. Kwa mujibu wa jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani, hadi Novemba mwaka jana watanzania 2,994 walikufa kwa ajali mbalimbali za barabarani za mabasi, malori, magari madogo, bajaji na bodaboda.
Ili kukabiliana na ajali hizo, jeshi hilo limekuwa likiendesha operesheni katika barabara zote kuu nchini kwa mfano kutumia tochi kukamata madereva wanaoendesha kwa mwendokasi au kwa uzembe.
Pia limekuwa likiwataka wananchi kushirikiana na polisi kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti ajali kwa mfano kutoa taarifa mara kwa mara wakiwa safarini, wanapobaini madereva wanaovunja sheria za usalama barabarani. Aidha limekuwa likihimiza wananchi kutoa ripoti katika vituo vya polisi juu ya madereva wanaofanya makosa.

Source: Sadick Hamidu

No comments:

Post a Comment