Wakazi wa Isanga Jijini Mbeya
wamekumbwa na taharuki baada ya tukio lisilo la kawaida ambapo maiti
iliyokwenda kuzikwa katika makaburi ya zamani ya Isanga ilikutwa ikiwa
kwenye godoro ndani ya nyumba alimofia.
Taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa
Mbeya inasema kuwa tukio lilitokea mnamo tarehe 16.01.2017 majira ya saa
4:30 asubuhi katika mtaa wa Igoma “A”, Kata ya Isanga, Jijini Mbeya.
Kufuatia taarifa hiyo Polisi
walifuatilia na kubaini kuwa tarehe 16.01.2017 majira ya saa 1:00
asubuhi mtu mmoja aitwaye JAILO KYANDO na mke wake aitwaye ANNA ELIEZA
wote wakazi wa mtaa wa Igoma “A” waliamka asubuhi na kukuta mtoto wao wa
kwanza aitwaye HARUN JAILO KYANDO amefariki dunia akiwa amelala.
Taarifa za awali zinadai kuwa marehemu
tangu utoto wake alikuwa na matatizo ya ugonjwa wa kifafa hali
iliyopelekea kuishi nyumbani pasipo kusoma.
Kufuatia kifo hicho msiba uliendeshwa
na taratibu za mazishi zilifanyika. Majira ya saa 6:00 mchana jeneza
lililetwa msibani na kuwekwa sebuleni kando ya mwili wa marehemu ambao
ulikuwa umeviringishwa na blanketi na kulazwa chini kwenye godoro, baada
ya maombi yaliyoongozwa na walokole waitwao BONDE LA BARAKA vijana
walibeba jeneza hadi makaburi ya zamani ya Isanga na kisha jeneza
kuzikwa.
Waombolezaji waliporudi nyumbani
walitaharuki kuona mwili wa marehemu mtoto HARUN JAILO KYANDO ukiwa
chumbani umelazwa eneo ulipokuwa awali.
Kutokana na hali hiyo taarifa
zilifikishwa Polisi mara moja, askari Polisi walifika na kurejesha hali
ya amani kwa kuuchukua mwili wa marehemu ambao kwa sasa umehifadhiwa
katika Hospitali ya Rufaa Mbeya.
Taratibu nyingine za mazishi
zitafanyika leo tarehe 17.01.2017. Mpaka sasa bado haijafahamika ni
uzembe /bahati mbaya wafiwa kusahau kuweka mwili wa marehemu kwenye
jeneza au kulikuwa na hujuma zozote.
Upelelezi unaendelea kuhusiana na tukio hili.
Source: Global Publishers
Source: Global Publishers
No comments:
Post a Comment