BAADA ya kudaiwa kulipwa fedha na kuingia mitini kwenye matamasha
mbalimbali, mwanamuziki ‘grade one’ wa nyimbo za Injili Bongo, Rose
Mhando (pichani) amenaswa akitumbuiza jukwaani akiwa na ujauzito mkubwa.
Tukio hilo lililowashangaza watu wengi lilitokea Jumapili iliyopita
katika Kijiji cha Ilongero jimbo la Singida Kaskazini kulipokuwa na
mkutano wa hadhara aliokuwa akiuhutubia Waziri wa Maliasili na Utalii,
Lazaro Nyalandu.
Wakati wananchi wakimsubiri Nyalandu ambaye pia ni mbunge wa Singida
Kaskazini ahutubie, zilitangulia burudani za hapa na pale ndipo baadaye
alipopanda Rose akiwa na kitumbo ‘ndii’ na kusababisha minong’ono chini
kwa chini.
“Mh! Jamani huyu ni Rose kweli au macho yangu? Si angepumzika? Mbona
tumbo tayari kubwa hivi, hata kama ni kusaka pesa lakini si kwa staili
hii, kuna wakati mtu inabidi fedha uzipe kisogo,” alisikika mmoja wa
wananchi.
Hata hivyo sambamba na watu kutilia shaka juu ya afya yake, Rose
alionekana kulimudu vyema jukwaa kwa kutumbuiza nyimbo zake huku akiimba
kwa staili ya kurukaruka kama kawaida.
Kwenye mkutano huo uliohudhuriwa na mamia ya wakazi wa Ilongero na jimbo
zima la Singida Kaskazini, mbali na kuzungumzia masuala mbalimbali ya
maendeleo, Nyalandu alitangaza nia ya kugombea urais mwakani.
No comments:
Post a Comment