MATANGAZO

/zest+mkali+3.jpg /TULAMCHA+2+copy.jpg

Wednesday, 4 December 2013

MAKOCHA WAZALENDO WAKUTANA KUPANGA MIKAKATI YA TANZANIA KUSHIRIKI AFCON 2015

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Kulia ni Meneja wa Bia ya Kilimnjaro, George Kavishe na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Kidau Alfred. 
Mdau wa Soka Shaffih Dauda (wa pili kulia) akiteta na makocha, Charles Boniface Mkwasa (kulia) na Kenny Mwaisabula ambao wamechaguliwa kuudhuria kikao maalumu kitakachofanyika mjini Zanzibar kuanzia Desemba 6 cha kupanga mikakati ya namna ya kuiwezesha Tanzania kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2015)

DAR ES SALAAM, Tanzania

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, ametangaza majina 17 kati ya 20 ya Jopo la Makocha Wazalendo watakaokutana kupanga mkakati wa namna ya kuiwezesha
Tanzania kushiriki Fainali za Mataifa Afrika (AFCON 2015) zitakazofanyika nchini Morocco.

Akizungumza na waandishi habari jijini Dar es Salaam, Malinzi alisema kuwa, makocha hao watakuwa na kikao maalumu (retreat) kitakachofanyika mjini Zanzibar kwa siku tatu kuanzia kesho Desemba 6 hadi 8, chini ya Mwenyekiti Kanali Mstaafu Idd Kipingu.

Malinzi aliwataja makocha wanaounda jopo hilo ambalo Katibu wake ni Pelegrinius Rutahyuga, kuwa ni Dk. Mshindo Msolla, Peter Mhina, Ayoub Nyenzi, Abdallah Kibadeni, Kidao Wilfred na Salum Madadi.

Makocha wengine waliotajwa na Malinzi kuwao katika jopo hilo ni pamoja na Juma Mwambusi, Kennedy Mwaisabula ‘Mzazi’, Boniface Mkwasa, Fred Minziro, Meja Abdul Mingange, Ally Mayay na Dan Korosso.

Malinzi alibainisha kuwa, kwa siku tatu makocha hao watakuwa na majadiliano ya namna gani Tanzania kupitia Taifa Stars inavyoweza kupata wachezaji wa timu za taifa za umri tofauti watakaowezesha mchakato wa kufuzu AFCON 2015 nchini Morocco.

“Nichukue nafasi hii kuwatakia kila la heri katika zoezi lao, litakalojumuisha makocha watatu kutoka Visiwani Zanzibar ambao watachaguliwa na chama cha soka cha huko (ZFA), kisha waje na majibu yatakayotuwezesha kufikia lengo,” alisema Malinzi.

Kwa upande wake, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager inayozalishwa na TBL, George Kavishe, alimshukuru Malinzi kwa hatua mbalimbali za kunyanyua soka alizoonesha tangu alipochaguliwa na kwamba TBL inajivunia hilo.

“Kama wadhamini wa Taifa Stars, TBL inapenda kumshukuru Malinzi kwa mkutano wake huu wa kwanza na sisi tangu alipochaguliwa, akishirikiana na Kamati ya Utendaji na tunaamini jitihada hizi zitadumu na kuzaa matunda,” alisema Kavishe.

Alienda mbali zaidi na kuwataka makocha waliochaguliwa kuunda jopo hilo maalum kutambua thamani ya jukumu lao na kuja na tiba sahihi ya matatizo yetu, huku wakitambua kwamba wako kamatini kwa niaba ya Watanzania zaidi ya milioni 45.

Aidha, Malinzi ameunda kamati mbili maalumu (ad hoc) kwa ajili ya kutathmini muundo wa ligi na kupendekeza namna ya kuuboresha, na ile ya kutahmini muundo wa Bodi ya Ligi na kupendekeza namna ya kuuboresha, ikiwemo kuunda kampuni.

Kamati ya Kutathmini Muundo wa Ligi inaongozwa na koocha wa zamani wa Taifa Stars, Dk. Mshindo Msolla, wakati Katibu ni Ofisa Mashindano wa TFF, Idd Mshangama. Wajumbe ni Rahim Kangezi, Amri Said, Sunday Manara, Salim Bawazir na Lucas Kisasa.

David Nchimbi kutoka Delloitte ataongoza Kamati ya Muundo wa Bodi ya Ligi, wakati wajumbe ni Edwin Kidifu (Mwanasheria wa SUMATRA), Jones Paul (Mkurugenzi wa Sunderland/Symbion Academy), Evans Aveva, John Jambele, Masoud Sanani na Pelegrinius Rutahyuga.

No comments:

Post a Comment