JESHI
la polisi nchini limefanikiwa kuisambaratisha ndoa ya mwanafunzi wa
kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Mboga iliyopo Chalinze
mkoani Pwani, Asha Daru mwenye umri wa miaka 15, aliyeozeshwa kwa Said
Ally (29), mkazi wa Pugu jijini Dar, Ijumaa iliyopita.
Ndoa
hiyo iliyotawaliwa na usiri mkubwa, ilifungwa nyumbani kwa bibi wa
mwanafunzi huyo aitwaye Asha Abdallah maeneo ya Tandale Kwamtogole, Dar.
Kuvuja
kwa siri ya ndoa hiyo kulifanikishwa na mmoja wa ndugu wa familia ya
mwanafunzi huyo ambaye alidai kitendo hicho kilimkera hivyo kuwaomba
mapaparazi wa Oparesheni Fichua Maovu (OFM) iliyo chini ya Global
Publishers kumnusuru binti huyo mdogo aliyedaiwa kulazimishwa kuolewa.
Baada
ya kumsikiliza kwa umakini ndugu huyo mwenye mvi za hekima, mapaparazi
wetu walilishirikisha jeshi la polisi na kuanza kuwafanyia mtego wa
kuwanasa waliokuwa wakifanikisha tukio hilo.
BWANA HARUSI AWASILI UKWENI
Mishale
ya saa 4:00 asubuhi kama ilivyoripotiwa na mtoa habari wetu, tayari
bwana harusi ambaye ni fundi seremala alikuwa akiwasili ukweni na
kupokelewa na nderemo za chinichini huku mapaparazi wetu wakiwa
wamezingira eneo hilo.
Mapaparazi
wetu walifanya upekepeke na kuingia hadi chumba cha bi harusi mtarajiwa
na kumkuta shangazi yake akimpamba fastafasta kwa kile ilichoonekana
kama walichelewa kumaliza kazi hiyo hadi ndoa inaanza kufungwa.
USTAADHI AMWAGA MAWAIDHA NA NDOA
Makachero
wa jeshi la polisi na OFM, wakiwa kama wageni waalikwa, walisubiri kila
kitu kiendelee ili kupata ushahidi wa tukio ambapo ustaadhi aliyekuwa
akifungisha ndoa hiyo alionekana akimfungisha Said ambaye alitamka mbele
ya waozaji na wageni wengine wakiwemo makachero kuwa anamuoa binti huyo
kwa mahari ya shilingi laki tatu na nusu ambapo alilipa laki mbili na
kubakiza deni la laki moja na nusu.
Baada ya tamko hilo, zilisikika nderemo za chinichini kutoka chumbani kwa bi harusi.
Huku
nderemo zikiendelea, ustaadhi aliyekuwa akifungisha ndoa hiyo alianza
kutoa mawaidha ya ndoa akiwausia maharusi kuishi kwa maadili ya
kumpendeza Mungu na kuijaza dunia kama watajaliwa.
POLISI WAVAMIA KATIKATI YA SHEREHE
Mambo
yakiwa yamenoga huku polisi wakisubiri wahusika wamalize mambo yao,
inspekta wa jeshi la polisi aliyevalia kiraia akiwa na ‘mkwaju kiunoni’
alisimama na kujitambulisha kwa jina la Inspekta Rodger na kuwaweka
chini ya ulinzi bwana harusi, ustaadhi, bi harusi, bibi yake na ndugu
wengine waliokuwa eneo hilo.
Wote
wakiwa chini ya ulinzi, Inspekta Rodger aliwatajia tuhuma zao na
kuwaita vijana wake waliotanda eneo hilo na kuwaamuru kuwakamata
watuhumiwa wote na kuwatia kwenye ‘difenda’ msobemsobe kwa ajili ya
safari ya kuelekea Kituo cha Polisi cha Magomeni, Dar kutoa maelezo.
MAHARUSI WATIWA KWENYE DIFENDA
Maharusi
waliongozwa na kupandishwa kwenye difenda na kufuatiwa na ustaadhi,
bibi wa bi harusi, mshenga aliyefahamika kwa jina la mama Batenga na
ndugu wengine.
BIBI AMWAGA TAMBO KITUONI
Wakiwa
kituo cha polisi, bibi wa bi harusi alikuwa akijigamba kuwa ndoa hiyo
ya mjukuu wake ni halali na kusema umri wa miaka 15 alionao siyo sababu
ya kukosa kuolewa. Akimzungumzia binti huyo mwanafunzi, bibi huyo
alisema aliamua kumuoza mjukuu wake huyo kwa kuwa alikuwa hapendi shule
na alikuwa amekubuhu kwa utoro hivyo akaona ni bora aende kwa mume.
“Kwani
mtu kuolewa na miaka 15 ni ajabu gani? Sisi Waluguru kwetu tunaolewa
hata chini ya miaka hiyo, mimi mwenyewe huyu babu yake amenioa nikiwa na
miaka 15, sasa leo ajabu iko wapi?” alihoji bibi huyo.
BWANA HARUSI ALALA LUPANGO
Ulipofikia
wakati wa kutoa maelezo, bwana harusi alisema kwamba yeye aliambiwa
mkewe mtarajiwa alikuwa na umri wa miaka 18 na angejua kama ana umri huo
asingemuoa.
Licha
ya utetezi huo, sheria iliendelea kumbana kwa kufanya kosa hilo ambapo
alifunguliwa kesi ya jaribio la ubakaji kisha akaswekwa lupango.
Wengine
waliowekwa rumande kwenye tukio hilo ni baba wa bi harusi, Daru
Abdallah, bibi wa bi harusi, Asha Abdallah, mjomba wa bi harusi ambaye
jina lake halikuweza kupatikana pamoja na mshenga.
Bi harusi huyo yeye alipelekwa ustawi wa jamii kwa ajili ya mchakato wa kuangalia mustakabali wa maisha yake.
No comments:
Post a Comment