Dar es Sakaam/Nairobi. Wakati
wa Jeshi la Polisi la Tanzania likisema linafuatilia taarifa za vitisho
za kundi la Al-Shabaab la Somalia za kushambulia, Mtanzania mmoja,
Vedasto Nsanzugwanko ambaye alijeruhiwa kwenye shambulio la Kenya
ameelezea yaliyomkuta.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba alisema
jana kuwa wameanza kufuatilia kwa undani taarifa zilizozagaa katika
mitandao ya kijamii kwamba kundi la Al-Shabaab linajipanga kuishambulia
Tanzania naUganda.
DCI Manumba alikiri kusikia taarifa hizo na kusema kuwa Jeshi la Polisi
limeanza kufanya uchunguzi wa kina: “Siwezi kukueleza ni uchunguzi wa
aina gani tutakaofanya, hiyo ni siri yetu.”
Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Meja Eric Komba alisema
kuwa kuna uwezekano taarifa hizo zikapikwa na wajanja wachache kwa
ajili ya kuwajengea hofu wananchi.
“Taarifa za kwenye mitandao wakati mwingine ni uzushi mtupu… kuna
kipindi ziliwekwa taarifa za uongo zinazohusu jeshi hili,” alisema.
Alipotakiwa kutoa msimamo wa jeshi hilo iwapo taarifa hizo zitakuwa na ukweli alisema, “Jeshi tuko tayari kwa jambo lolote.”
Mtanzania ajeruhiwa
Nsanzugwako ambaye ni Meneja wa Kitengo cha Kulinda Watoto kwenye
Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Watoto (Unicef), Kenya
alisema kwamba akiwa katika Hospitali ya Aga Khan, Nairobi alipigwa
risasi miguu yote miwili.
Alisema alifikwa na mkasa huo baada ya kupitia katika maduka hayo
akitokea kazini ili kupata kahawa... “Nilipofika baada ya nusu saa
nilisikia milio ya risasi ndipo nikaona purukushani zimeanza.”
Nsanzugwako alisema alianza kukimbia na wenzake huku wakijaribu kuokoa
watoto waliokuwepo katika eneo hilo ambao walikuwa katika shindano la
mapishi lililoandaliwa na Radio Africa Group.
“Watoto walianza kukimbilia ghorofa za juu zaidi na magaidi walianza kuwafuata.
“Baada ya hapo, waliendelea kutukimbiza
na nilikutana nao ana kwa ana na mmoja wa magaidi hao ambaye
alinifyatulia risasi na kunipiga miguu yote miwili,” alisema
Alieleza kwamba alijikongoja hadi
alipofanikiwa kutoka nje kwa kupitia mlango uliokuwa mbele yake na
kupokewa na polisi na kisha kuchukuliwa na Msalaba Mwekundu kwa ajili ya
huduma ya kwanza na kisha kupelekwa hospitalini kwa matibabu.
“Jioni yake nilitakiwa kusafiri kwenda Geneva, Uswisi kikazi lakini kutokana na tukio hilo nilishindwa kufanya hivyo,” alisema.
Alisema amekuwa jijini Nairobi kwa miezi saba akiwa anafanya kazi Unicef.
Kaka wa majeruhi huyo, Mbunge wa zamani
Kasulu Mashariki, Daniel Nsanzugwako, alisema amekuwa akiwasiliana na
mdogo wake huyo na kwamba anaendelea vyema.
Nsanzugwako, ambaye aliwahi kuwa Naibu
Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo alisema mdogo wake alimweleza
kuwa tayari ameshafanyiwa upasuaji lakini bado hajaweza kutembea.
Taarifa iliyotolewa jana na Ofisa wa
Ubalozi wa Tanzania nchini Kenya, Shiyo Innocent ilithibitisha kuwapo
kwa Mtanzania mmoja ambaye amejeruhiwa kwa risasi katika miguu yake
yote... “Ubalozi unaendelea kufuatilia kama kuna Watanzania wengine
waliokuwepo kwenye tukio hilo.”
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nchi
za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John Haule alisema Serikali
inaendelea kufuatilia afya ya Mtanzania huyo.
“Ofisi yetu ya ubalozi iko karibu na
inafuatilia kila kinachoendelea. Kwa sasa nimeambiwa kuwa majeruhi
anaendelea vizuri na tuna matumaini atapata ahueni,” alisema.
chanzo:mwananch
No comments:
Post a Comment