MATANGAZO

/zest+mkali+3.jpg /TULAMCHA+2+copy.jpg

Thursday, 8 August 2013

UONGOZI WA SIMBA WAMLALAMIKIA WAKALA WA MCHEZAJI OLOYA


UONGOZI wa klabu ya Simba umesema wakala wa mshambuliaji, Moses Uloya ndiye anayekwamisha mipango yao ya kumsajili mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uganda.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, wanahisi wakala huyo anafanya mipango ya kumuuza mchezaji huyo kwa klabu nyingine.

Hanspope alisema kutokana na kuingiwa na wasiwasi huo, wameamua kumsubiri Oloya amalize mkataba wake uliosalia wa kuichezea klabu ya  XI Mang Saigon ya Vietnam.

Oloya, ambaye anadaiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa Simba na Yanga, amesaliwa na mwezi mmoja kumaliza mkataba wake na XI Mang Saigon. Mkataba huo unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi huu.

"Tulishazungumza na Oloya na kukubaliana naye kwamba, tusubiri amalize mkataba wake huko Vietnam, lakini wakala wake anataka tuilipe klabu yake malipo ya kuvunja mkataba ili atue Simba,"alisema Hanspope.

"Kutokana na kubaini ujanja huo, tumeamua kusubiri mkataba wake utakapomalizika ndipo tufanye mipango ya kumsajili akiwa mchezaji huru. Hatuwezi kuilipa klabu yake fedha za kuvunja mkataba wakati zimesalia siku chache," aliongeza mfanyabiashara huyo.

Simba imeelezea msimamo wake huo baada ya klabu ya Yanga kuripotiwa kuwa, imeamua kujitosa katika vita ya kumsajili mshambuliaji huyo kwa kumtengea kitita kikubwa cha pesa.

Simba na Yanga zimeripotiwa kutenga nafasi moja kwenye usajili wake, zikimsubiri
mchezaji huyo. Klabu zote mbili zimepanga kufanya usajili huo wakati wa dirisha dogo.

Alipoulizwa jana kuhusu mipango ya Yanga kumsajili mshambuliaji huyo, Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya klabu hiyo, Abdalla Bin Kleb alisema hawana mpango huo.

"Tuna mambo mengi sana ya kufanya na  sijui lolote kuhusu Oloya,"alisema Bin Kleb.

No comments:

Post a Comment