MWANAMKE maarufu duniani, Oprah Winfrey amekumbana
na kitendo cha ubaguzi wa rangi nchini Switzerland baada ya muuza duka
mmoja kukataa kumuuzia mkoba wa kike wa mkononi na kumwambia kuwa
asingeweza gharama yake. Oprah ambaye ametajwa katika vitabu vya
‘Forbes’ kama mwanamke mwenye ushawishi mkubwa wa kisiasa duniani na
mmoja wa watu matajiri zaidi amedai kuwa muhudumu wa kisichana aliyekuwa
akiuza katika duka moja alimdharau kutokana na rangi yake.
Uswis imejikuta ikiwa gumzo kwa wanaharakati wa haki za binadamu,
kwani wiki iliyopita nchi hiyo ilitangaza sheria kuwa wahamiaji wa nje
hawataruhusiwa kushirikiana na raia wenyeji hasa katika maeneo ya umma
kama vile mabwawa ya kuogelea, uwanja wa michezo na hata kanisani.
Sasa madai ya Oprah yanatoa taswira mbaya zaidi ya jinsi hali ilivyo
nchini humo kuhusu ubaguzi wa rangi. Wanaharakati wa haki za binadamu
wamesema kuwa hii ni ishara ya kuwa na ubaguzi ule uliowahi kutokea kwa
muda mrefu huko Afrika Kusini. Oprah alisema aliamua kuondoka dukani
hapo taratibu bila kufanya vurugu lakini amesikitishwa kuona kuwa bado
ubaguzi wa rangi unaendelea na kuenea.
Mwaka jana pekee Oprah alikuwa na fedha jumla ya dola za Kimarekani
milioni sabini na saba na amesifiwa kuwa mfanyibiashara tajiri, ambaye
pia anamiliki shirika lake binafsi la utangazaji na anafadhili miradi
mingi ya misaada katika maeneo anuai duniani.
Alipata umaarufu wake kutokana na kipindi chake cha Oprah Winfrey
Show kinachooneshwa nchi nyingi. Hata hivyo mwandishi wa BBC mjini
Zurich anasema kuwa kipindi hicho hakijawahi kupeperushwa katika runinga
za Switzerland na huenda sio wengi wanaomfahamu Oprah ni nani. Oprah
alikwenda Uswis kuhudhuria harusi ya mwanamuziki Tina Turner.
-BBC
No comments:
Post a Comment