Ana sifa nyingi, lakini iliyo kubwa ni ucheshi, uchangamfu, ukarimu na
kila aina ya bashasha. Hata hivyo kwa sasa hali yake ni tofauti, mambo
mengi yamebadilika.
Sipati shida kumpata pale nilipokusudia kumfikia na hata ninapofika
nyumbani kwake katika banda la vyumba viwili ambavyo vimemalizwa
kujengwa hivi karibuni, napokewa na msichana anayenikaribisha katika
kiti nje ya kibanda hicho.
Ujumbe unapelekwa ndani kwa Mzee Small kuwa ana mgeni na dakika 20
baadaye mlango unafunguliwa, anachomoza mtu ambaye sipati taabu
kumfahamu kuwa ni Mzee Small, mwigizaji nguli ambaye maradhi
yamemkalisha kitako.
Anachechemea huku mkono wa kushoto akiwa ameufumbata kwapani, uso umekumbwa na maumivu yanayoshindana na tabasamu
hafifu analojaribu kulitoa.
Hali hiyo inaakisi wimbo mmoja wa Shakila Abdallah
‘Bi. Shakila’ wenye mashairi ‘Macho yanacheka moyo unalia’. Kimsingi
Mzee Small anaumwa ingawa anajaribu kutabasamu, kinachoonekana katika
paji lake la uso ni tofauti na tabasamu hafifu analojaribu kulitoa pale
macho yetu yanapogongana na wakati wa mazungumzo anabainisha
kinachomsibu.
“Sipo vizuri, naumwa. Kwa sasa inawezekana ikaonekana kama nina nafuu
kidogo, lakini naumwa,” anasema baada ya kunikaribisha katika chumba
kimoja ambacho anakimiliki na mkewe.
Chanzo cha tatizo
Anasema tatizo lake lilimuanza Mei mwaka jana baada ya kurudi kutoka
Mwanza alikokuwa na kazi ya kutumbuiza katika tamasha la kupambana na
mauaji ya Albino. Tamasha hilo liliratibiwa na Kituo cha Under The Same
Sun .
“Nilitoka Uwanja wa Ndege (Dar es Salaam) na kufika hapa nyumbani,
nikaingia chooni moja kwa moja. Lakini wakati natoka, nikadondoka.
Nilipojitahidi kunyanyuka haikuwezekana hivyo nikabebwa hadi chumbani,”
anasema.
Anasema akiwa chumbani alijaribu kujinyanyua akajikuta anadondoka tena,
hivyo akawahishwa hospitali moja jirani na nafuu haikupatikana.
Ikalazimika apelekwe Hospitali ya Amana jijini Dar
es Salaam ambako alilazwa siku tatu kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Anasema alikaa Muhimbili mwezi mzima bila matibabu ya maana na baadaye
akaruhusiwa kurudi nyumbani baada ya kupewa dawa chache. Lakini akiwa
tayari amepooza mkono na mguu, vyote upande wa kushoto.
Mzee Small anasema matibabu katika hospitali hiyo hayakuwa ya kueleweka
na pengine kwa kuwa hakuwa na fedha za kutosha basi hakuna aliyemjali.
“Baada ya kurudi nyumbani niliamua kuhangaika na mambo ya ‘Kiswahili’
(waganga wa jadi) kwani niliambiwa kuwa ule ni ushirikina kwani kuna mtu
alileta kitu na kukichimbia mlangoni kwangu na
kingine nje ya choo, hivyo nikaingia katika tiba mpya,” anasema.
Anabainisha kuwa ‘mafundi’ wengi walimtembelea nyumbani kwake na kila
aliyekuja alimweleza kuwa sasa tatizo lake limeisha na kumpa dawa
zikiwamo za kuchua. Hata hivyo anasema hakukuwa na jipya zaidi ya
kumaliza tatizo la kizunguzungu lililokuwa likimsumbua pia.
“Kweli kizunguzungu kilichokuwa kinanikabili kiliisha, lakini bado mguu
na mkono vimebaki vimepooza hadi sasa,” anasema na kuongeza kuwa mbaya
zaidi waganga hao kila mmoja kwa wakati wake walihitaji fedha.
Anasema wa mwanzo alimwambia akitoa Sh 300,000 atapona, aliyefuata
alihitaji Sh 200,000 fedha ambazo alijitahidi kuzitoa baada ya kuuza
sehemu ya shamba lake eneo la Kiparang’anda, lakini hakupata nafuu.
Anasema kuna ‘Fundi’ mmojawapo alitoka Kigoma na hivyo akalazimika
kumpatia hadi chumba cha kulala, lakini ‘fundi’ huyo alitoweka baada ya
mgonjwa wake mwingine aliyekuwa eneo la Segerea, Dar es Salaam kufariki
wakati anahudumiwa na ‘fundi’ huyo.
“Kuna mgonjwa alienda siku ya kwanza akamchukulia dawa zake, akarudi
tena siku ya pili, alipofika siku ya tatu akakuta maturubai na watu
wamejaa. Yule mganga akageuza njia na hakurudi tena huko na aliniaga
kuwa anarudi kwao,” anasema Mzee Small.
Anasema tiba za mganga huyo zilimtia shaka na ilifika wakati alizikataa kabisa.
“Nilimwambia mimi basi inatosha ila kama kuishi katika mazingira haya
wee kaa tu ila kwa tiba zako mimi basi tena, lakini mganga huyo
aliendelea kung’ang’aniza hadi tukio hilo la Segerea ambalo lilimkimbiza
mjini,” anasema.
Mzee Small anasema amelazimika kuuza shamba ili aendelee na matibabu na kumalizia sehemu ya kibanda chake anachoishi sasa.
Kuhusu tatizo lake, anasema mkono uliopooza sasa unaonyesha kuanza kutengana na bega.
“Sijui hasa ni nini, nina wasiwasi huenda kuna tatizo jipya
linajitengeneza. Yaani nimebaki kumwomba Mungu anisaidie kuninusuru na
ugonjwa huu,” anasema kwa masikitiko makubwa.
“Nipo njiapanda na sielewi tatizo ni nini. Kibaya zaidi sasa hata ndugu
zangu wamenitenga. Hakuna hata mmoja ambaye anashughulika na afya yangu
wala kujaribu kunijulia hali.”
Anasema siku za awali ndugu hao walijitokeza na kumjulia hali, lakini kadiri siku zilivyoenda wakaanza kukacha.
“Ndugu pekee aliyebaki sasa ni mke wangu, vyombo vya habari na baadhi ya mashabiki ambao hufika hapa,” anasema.
Mzee Small ambaye ametamba katika vikundi mbalimbali vya maigizo na
vichekesho na kujizolea umaarufu mkubwa ambao ulimwezesha kupata
mikataba na kampuni kadhaa mbali ya maonyesho ya jukwaani, anasema mambo
yake sasa si shwari kabisa.
Read more: http://talkbongo.blogspot.com/2013/07/afya-ya-mzee-small-yazidi.html#ixzz2ZbEUblmw
No comments:
Post a Comment