MATANGAZO

/zest+mkali+3.jpg /TULAMCHA+2+copy.jpg

Saturday, 20 July 2013

MIILI YA WANAJESHI WA TANZANIA (JWTZ) WALIOUWAWA DARFUR KUWASILI LEO.

 
MIILI ya askari saba wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), waliofariki dunia katika Jimbo la Darfur nchini Sudan, inatarajiwa kuwasili nchini leo saa 9 alasiri. Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Habari na Mahusiano makao makuu ya JWTZ jana, ilisema miili hiyo itawasili 9 na si saa 4 asubuhi kama ambavyo ilitangazwa juzi.

Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano, Meja Joseph Masanja alisema miili itawasili kwa ndege maalumu katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Baada ya kuwasili, itapelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Lugalo kuhifadhiwa, wakati maandalizi ya kuiaga kitaifa yakiendelea.

“Miili hii, itawasili kwa ndege maalumu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Terminal one (Air Wing) saa 9 alasiri Julai 20, 2013, badala ya saa 4 kama ilivyoelezwa awali, waandishi wa habari wanaruhusiwa kufika kuanzia saa 7 mchana.

“Tunategemea miili yote, itaagwa kwa heshima zote Julai 22, 2013 kuanzia saa 3:00 asubuhi katika viwanja vya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Upanga,” ilisema taarifa hiyo.

Tukio la askari hao kuuawa, lilitokea Jumamosi iliyopita katika Jimbo Darfur nchini Sudan, wakati askari hao wakiwasindikiza waangalizi wa amani.

Askari hao, walishambuliwa umbali wa kilomita 20 na kundi la watu ambao hawajajulikana mpaka sasa.

Baada ya tukio hilo, Rais wa Sudan, Omar Bashir alifanya mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete kwa njia ya simu na kuahidi kuwasaka watu wote waliohusika.

Jumla ya askari 875 wa Tanzania, walipelekwa Sudan kulinda amani katika Jimbo la Darfur kwa kushirikiana na vikosi vya Umoja wa Mataifa.

No comments:

Post a Comment