MAMA ANNA MKAPA.
MKUTANO wa wake za marais uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wazito, akiwemo Rais wa zamani wa Marekani, George W. Bush na Mkewe, Laura, umeacha kitendawili kizito kuhusu mke wa Rais wa zamani, Benjamin Mkapa, Mama Anna Mkapa. Imebainika kuwa katika mkutano huo, ambao mke wa Rais Jakaya Kikwete, Salma alikuwa ni mwenyeji wao, Mama Anna Mkapa hakuhudhuria, lakini pia imeonyesha wazi kwamba hakupewa fursa kulingana na hadhi yake.
Mkutano huo wa Kimataifa ulifanyika katika Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam, Juni 2-3 mwaka huu, uliozungumzia nafasi ya wanawake kuinuka kimaendeleo, ukizihusisha taasisi zinazoendeshwa na wake wa marais, wakiwemo wale wastaafu.
Gazeti hili lilibaini kuwa, katika mkutano huo kiligawiwa kitabu kilichobeba jina la ‘African First Ladies Summit’, kilichokuwa na orodha ya viongozi mbalimbali, wakiw
emo wake za marais na wake za marais wastaafu takribani 31, kikielezea wasifu na taasisi wanazoziongoza, lakini Jina la Mama Mkapa halikuwemo.
Katika kitabu hicho, Mama Mkapa, ambaye anaendesha Taasisi ya Fursa Sawa Kwa Wote (EOTF), jina lake kutokuwepo, baadhi wanaona kwamba Mkutano huo haukumpa fursa mama huyo, hasa kutokana na kazi kubwa ambayo imekuwa ikifanywa na taasisi yake hiyo ya kuwainua wanawake kama mazungumzo ya mkutano huo yalivyokuwa yameegemea.
Taasisi ya EOTF ni taasisi ya kwanza kuendeshwa na mke wa Rais hapa nchini, na ilianzishwa wakati Rais Benjamin Mkapa akiwa madarakani. Tangu ilipoanzishwa imekuwa ikijishughulisha na kuwainua wanawake kiuchumi kupitia shughuli mbalimbali, ikiwemo ujasiriamali.
Tofauti na mama Anna Mkapa ambaye haijulikani kama alitengwa au alijitenga katika mkutano huo, lakini kitabu hicho kilielezea wasifu na shughuli zinazofanywa na wake za marais kama Mama Salma kupitia taasisi yake ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), Mke wa Rais Obama, Michelle ambaye juhudi zake amezielekeza katika kujenga jamii na familia kupitia mradi wake wa Let’s Move!.
Wengine ni pamoja na mke wa Waziri Mkuu wa zamani Tony Blair, Cherie Blair, Laura Bush na wengine.
MTANZANIA Jumapili lilimtafuta kwa njia ya simu msaidizi wa Mama Mkapa aliyetambulika kwa jina moja la Prisca, ambaye alikiri kuwa alipata mwaliko wa mkutano huo.
Kuhusu kutohudhuria, alisema hilo lilitokana na programu zake nyingi, ikiwa ni pamoja na banda ndani ya viwanja vya maonyesho ya kimataifa ya 37 ya biashara, Sabasaba ambako alikuwa na wageni wake.
Alipoulizwa mbona mkutano huo ni mkubwa sana huku Mama Salma pia akiwa na banda lake huko, lakini aliliacha na kwenda katika Mkutano, iweje kwa mama Mkapa, Prisca alisema hilo limetokana na kuwa na ‘programu’ zake nyingine.
Prisca alipoulizwa kama Mama Mkapa alialikwa katika mkutano huo, alisema kualikwa si tatizo, kwani anaweza kualikwa, lakini akawa na mambo mengine.
Alipoulizwa kama kuna tatizo kati ya EOTF na WAMA, alieleza kuwa hakukuwa na tatizo lolote, kwani hata katika kumpokea Mama Obama wakati alipotembelea ofisi za WAMA, Mama Anna Mkapa alikuwepo.
Prisca alisema kuwa hakuna tatizo kwa kuwa Mama Salma ni mke wa rais na Mama Mkapa alikuwa mke wa rais, hivyo hawana cha kugombea.
“Mama Salma akimwita Mama (Anna) kwenye ‘programu’ zake huwa anakwenda, vivyo hivyo kwa mama anapomwita mama Salma.
“Ninyi waandishi mambo madogomadogo kama hayo muwe mnayaacha na ndiyo yanawaweka katika matatizo na familia zenu, Mama Salma na Mama Mkapa wote wako ‘busy’ na hivi vitu naomba viishie hapo… kwanza umepata wapi namba yangu?” Alihoji Prisca.
Mkutano huo wa wake za marais, mbali na kuhudhuriwa na mke wa Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Cherie Blair, ulihudhuriwa pia na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Ukimwi (Unaids), Michel Sidibé.
Baadhi ya wake za marais waliohudhuria pia ni pamoja na Mke wa Rais wa Uganda, Janet Museveni, mke wa Rais wa Msumbiji, Maria da Luz Dai Guebuza, mke wa Rais wa Sierra Leone, Sia Nyama Koroma, Balozi Nancy G. Brinker ambaye ni kiongozi wa kimataifa wa kupambana na ugonjwa wa kansa pamoja na wengine wengi.
No comments:
Post a Comment