Watoto wawili wakiume wamekufa na mmoja kunusurika baada ya
kulipukiwa na kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu eneo la Jeshi la
Wananchi nchini (JWTZ) huko Kimbiji, Kigamboni.
Watoto hao wanaotoka katika familia tofauti wenye umri wa miaka
nane na kumi walikutwa na mkasa huo juzi wakati wakiwa wanacheza maeneo
hayo.
Mmoja wa ndugu wa marehemu ambaye hakutaka jina lake liandikwe
gazetini, aliliambia NIPASHE kuwa, eneo la tukio kulikuwa na watoto
watatu akiwamo mwenye umri wa miaka mitano ambaye alinusurika kwenye
mlipuko huo.
Alimtaja mtoto aliyefariki kwa jina moja kuwa ni Yohana.
Akisimulia zaidi ndugu huyo alisema siku ya tukio watoto hao,
walitoka nyumbani kuelekea eneo hilo la jeshi ambalo wanajeshi hulitumia
kwa mazoezi ya kijeshi.
“Huwezi amini kutoka hapa nyumbani hadi huko walikolipukiwa ni mbali,
yaani sijui walifikaje, ila ndiyo michezo ya watoto,”alisema.
Alieleza kuwa, watoto hao wakiendelea na michezo yao, walimuona nyani na kuanza kumkimbiza.
Alisema baada ya kufika maeneo hayo ya jeshi waliona kitu kama gololi na kukiokota.
“Baada ya kuikokota wakaanza kunyang’anyana ndipo ulipotokea mlipuko
na kuwajeruhi na kuwaua watoto wawili mmoja akiwa ni Yohana, yule wa
miaka mitano aliokoka na kurudi nyumbani kuwajulisha kile kilichowatokea
wenzake,” alisema.
Aidha, kutokana na tukio hilo miili ya watoto hao inaendelea kufanyiwa uchunguzi wa kina na inatarajiwa kuzikwa wiki ijayo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, Kamishina Msaidizi wa Polisi
(ACP), Engelbert Kiondo, alipopigiwa simu kuhusiana na tukio hilo, awali
aliahidi kulifuatilia lakini baadaye alipopigiwa, ilipokelewa na
mwanamke na kudai siyo ya kamanda.
Baadhi ya matukio ya milipuko au kuleta taharuki baada ya wananchi
kufananisha chuma na bomu ni pamoja na Januari 2, mwaka huu taharuki
ilitokea eneo la makutano ya barabara ya Morogoro na Shekilango, baada
ya kuonekana kitu kilichofananishwa na bomu la kutupwa na mkono.
Tukio hilo lilisababisha wakazi wa eneo hilo, wafanyabiashara, wapita
njia kupata hofu lakini baada ya polisi kulifanyia uchunguzi walibaini
siyo bomu.
Aidha, kwa mwaka jana kuanzia mwezi Septemba, matukio yaliyotokea ni
pamoja na lile la wanafunzi wawili wa kidato cha kwanza, katika shule
ya Sekondari Matombo mkoani Morogoro, kunusurika kufa baada kulipukiwa
na kujeruhiwa na kitu kilichosadikiwa kuwa ni bomu wakati wakitoka
shule.
Mwezi Oktoba watoto wengine watatu wakazi wa Kijiji cha Likombora,
Kata ya Mihumo wilayani Liwale, Mkoa wa Lindi walifariki baada ya
kulipukiwa na kitu kinachosadikiwa kuwa bomu.
Tukio lilitokea ikiwa imepita wiki, baada ya mgambo wakiongozwa na
mshauri wao, Meja Tiba kufanya mazoezi ya kulenga shabaha ya silaha huko
kwenye Kijiji cha Kipule ambako mabomu matatu hayakulipuka na
wakafanikiwa kuyaokota mawili na kuyateketeza.
Mwaka juzi katika kijiji cha Rugarama Kata ya Iyande wilaya ya
Karagwe mkoani Kagera, watoto watano walikufa baada ya kulipukiwa na
bomu la kutupa kwa mkono walilookota wakati wakikusanya vyuma chakavu.
–NIPASHE–
No comments:
Post a Comment